Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel amesema kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha dawa za kufubaza makali ya virusi vya Ukimwi (ARV) zinapatikana bure kwa wagonjwa nchini Tanzania.
Dk. Mollel ameyasema hayo wakati akishiriki katika uzinduzi wa awamu ya tatu ya mradi wa Timiza Malengo uliofanyika Mkoani Lindi uliozinduliwa na Naibu Waziri wa ofisi ya Waziri Mkuu, Ummy Deriananga kwa niaba ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa.
“Serikali itaendelea kufanya kila juhudi kuhakikisha kwamba huduma za afya zinawafikia watanzania wote bila ubaguzi ikiwa ni pamoja na dawa za kufubaza makali ya virusi vya Ukimwi (ARV) zaidi ya Shilingi bilioni 48 imewekezwa kuboresha miundombinu ya afya jambo la msingi ni wananchi kujenga utamaduni wa kupima afya ili kuepuka magonjwa,” amesema Dkt Mollel.
Mradi wa Timiza Malengo utatekelezwa kwenye Halmashauri 36 za Mikoa 10 lengo likiwa kuboresha huduma za afya maeneo ya vijijini.