Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, amesisitiza umuhimu wa Vyuo vya VETA kutoa mafunzo yanayokidhi mahitaji halisi ya soko katika jamii.
Akizungumza Machi 18, 2025, jijini Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 30 ya VETA, Waziri Mkuu ameeleza kuwa tafiti za kina zinahitajika ili kubaini mahitaji halisi ya ujuzi kulingana na shughuli za kiuchumi na kijamii.
Waziri Mkuu ameitaka VETA kuhakikisha kuwa wanatoa mafunzo yanayosaidia kuboresha ustawi wa jamii.
Ameeleza kuwa kujifunza maarifa ya kiufundi yanayohusiana na mazingira halisi ya kazi kutasaidia sana kuongeza tija na kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira nchini.
Akizungumza mabadiliko ya kiteknolojia, Waziri Mkuu amesisitiza umuhimu wa VETA kuhimiza matumizi ya mbinu za kidijitali ili kuwapa wanafunzi ujuzi wa kisasa utakaowawezesha kuendana na mahitaji ya ulimwengu wa sasa unaobadilika haraka na kuhakikisha kuwa vijana wanapata elimu bora na yenye tija.
Waziri Mkuu alihitimisha kwa kuhimiza VETA kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta binafsi na viwanda pamoja na kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanakidhi vigezo vya kimataifa. Hii itawezesha wahitimu wa vyuo vya VETA kushindana kimataifa katika soko la ajira.