Kampuni ishirini za uwekezaji kutoka Japan zipo nchini kutazamia fursa katika sekta za kilimo, utalii, na uzalishaji wa viwandani, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha mahusiano kati ya nchi hizi mbili.
Kampuni hizi zimekutana na makampuni 50 za Kitanzania kubadilishana uzoefu, kushirikiana katika teknolojia, na kuendeleza miradi ya pamoja ya kibiashara, ambayo hatimaye itaimarisha uchumi wa nchi na kuongeza ajira kwa wananchi.
Wawekezaji hawa wa Japan wamekuja wakati ambapo jumla ya thamani ya uwekezaji wa Kijapani katika kipindi cha miaka 12 iliyopita imefikia zaidi ya dola milioni 11.4 (zaidi ya Sh28.8 bilioni) katika miradi 24 iliyosajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na kufanikiwa kuunda zaidi ya ajira 1,000.
Akizungumza katika ufunguzi wa Kongamano la Uwekezaji na Biashara kati ya Tanzania na Japan jana, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Exaud Kigahe, alielezea umuhimu wa hatua hii kwa sekta ya uwekezaji nchini Tanzania.
“Tanzania na Japan zina mahusiano ya muda mrefu katika biashara, hususan katika miradi ya maendeleo kwenye sekta za viwanda na barabara,” alisema.Alibainisha kuwa Japan inaendelea kuwa mshirika mkuu wa maendeleo, ikisafirisha bidhaa kama magari na vifaa vya kielektroniki, huku Tanzania ikisafirisha malighafi na bidhaa za kilimo, zikiwemo bidhaa zilizoongezwa thamani kama chai na kahawa.