Ujerumani imesitisha msaada mpya wa maendeleo kwa Rwanda na inakagua ahadi zake za awali kutokana na mchango wa taifa hilo katika mgogoro unaoendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wizara ya maendeleo ya Ujerumani ilitangaza Jumanne.
Kwa kushirikiana na washirika, Ujerumani itaendelea kupunguza ushirikiano wa pande mbili na Rwanda,” ilisema taarifa hiyo, ikiongeza kuwa Berlin iliiarifu Rwanda mapema kuhusu hatua hiyo na kuitaka iachane na kuunga mkono kundi la waasi la M23, ambalo limepata mafanikio makubwa mashariki mwa Kongo.Kulingana na wizara hiyo, Ujerumani iliahidi msaada wa dola milioni 98 kwa Rwanda mnamo Oktoba 2022 kwa kipindi cha 2022 hadi 2024.
Rwanda inakabiliwa na shinikizo la kimataifa kutokana na madai kuwa inaunga mkono kundi la M23, ambalo tangu Januari limeiteka sehemu kubwa ya mashariki mwa Kongo pamoja na maeneo yenye rasilimali za madini ya thamani.
Mashambulizi hayo yanayoendelea ni kuzorota kwa kiwango kikubwa zaidi kwa mgogoro wa muda mrefu unaotokana na athari za mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994 na mapambano ya kudhibiti utajiri wa madini wa Kongo.
Kongo, wataalamu wa Umoja wa Mataifa, na mataifa ya Magharibi wanaishutumu Rwanda kwa kuunga mkono kundi hilo. Rwanda inakanusha tuhuma hizo na inasema inajilinda dhidi ya wanamgambo wa Kihutu walio na lengo la kuwaua Watutsi waliopo Kongo na wanaoitishia Rwanda.