Tanzania imefikia hatua ya kihistoria kwa kupata zaidi ya Sh1.52 trilioni kutokana na mauzo ya korosho nje ya nchi katika msimu wa 2024/25, baada ya kuzalisha tani 528,260 za korosho ghafi (RCN).
Kwa mujibu wa Taarifa ya Mapitio ya Kiuchumi ya Kila Mwezi ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya Februari 2024, mapato ya awali, ambayo ni sawa na dola milioni 583.7, yanaonyesha kuwa takwimu za mwisho huenda zikazidi dola milioni 600.
Hii ni ongezeko kubwa ikilinganishwa na mapato ya msimu uliopita ya dola milioni 221.3 (Sh575 bilioni) yaliyotokana na tani 254,500 za korosho ghafi. Takwimu hizi mpya zimevunja rekodi ya awali ya Tanzania iliyowekwa katika msimu wa 2017/18, ambapo dola milioni 575 zilipatikana kutokana na tani 313,000 za korosho ghafi.
Mapato ya korosho yamekuwa yakibadilika katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, ambapo mwaka 2022 yalifikia dola milioni 180.6 kutokana na tani 240,158, huku mwaka 2021 yakifikia dola milioni 282.1 kutoka tani 210,786.
Mavuno makubwa ya msimu wa 2024/25 yamechangiwa na usafirishaji wa tani 410,000 kupitia minada, huku tani 118,262 zikichakatwa ndani ya nchi kwa matumizi ya ndani na soko la kimataifa.
Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) inahusisha ongezeko hili la uzalishaji na ruzuku za serikali, ambazo zilihusisha usambazaji wa tani 41,263 za unga wa salfa na lita milioni 2.7 za viuatilifu vya kimiminika kwa wakulima.