Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa amesema Reli ya Kisasa ya Umeme (SGR) ikikamilika Mkoa wa Mwanza utakuwa kitovu cha biashara kanda ya ziwa.
Kadogosa ameyasema hayo jana usiku Jumanne Machi 18, 2025 katika hafla iliyofanyika jijini humo kuangazia miaka minne ya Rais Samia Suluhu Hassan madarakani.
Mkoa huo unaunganishwa na SGR kwa kipande cha Isaka -Mwanza chenye urefu wa kilomita 341 ambacho kinajengwa kwa gharama ya Sh3.06 trilioni na hadi mwezi huu ujenzi wake umefikia asilimia 63.04
“Miliyoyaona kanda ya ziwa ni yaliyotendeka na yanayoendelea kutendeka katika ujenzi wa reli, tunazungumzia miaka minne ya Rais Samia, kwa sisi watu wa ukanda huu lengo tunalijua, mradi huu ukikamilika Mwanza itakuwa kitovu cha biashara,” amesema Kadogosa.
Katika hafla hiyo mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ambaye amesisitiza mradi huo utakamilika na kuwanufaisha wakazi wa ukanda huo.
“Reli imeanza (SGR) na mchakato wa ujenzi katika vipande vingine unaendelea, endeleeni kumuamini Rais wetu ilimradi tuliapa kuwasaidia, tutawatumikia na mtanufaika na mradi huu” amesema Majaliwa.