Dar es Salaam, Machi 18, 2025 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema kuwa dhamira ya Serikali ni kukamilisha ujenzi wa Vyuo vya VETA katika wilaya ambazo hazikua na vyuo hivyo.Hatua hii inalenga kuwawezesha Watanzania kupata stadi na ujuzi muhimu kwa ajili ya kupunguza changamoto za ajira nchini.
Akizungumza katika uzinduzi wa Maadhimisho ya miaka 30 ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Prof. Mkenda ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha mfumo wa mafunzo ya ufundi na ufundi stadi (Amali) kwa kuunganisha majukumu ya urekebu wa mafunzo hayo iliyokuwa ikifanywa ma VETA na NACTE Hatua hiyo imezalisha Taasisi ya moja ya urekebu ya NACTVET.
Alisisitiza kuwa ushirikiano na kati ya VETA na wazalishaji na viwanda utaendelea kuimarishwa ili wanafunzi wapate ujuzi halisi kutoka viwandani kulingana na fani wanazosoma.
Aidha, Prof. Mkenda alibainisha kuwa serikali imekuwa ikitoa ruzuku kwa vyuo vya VETA, hatua ambayo imewezesha ada kuwa nafuu. Wanafunzi wa bweni wanalipa ada ya shilingi 120,000 tu kwa mwaka, huku wale wa kutwa wakilipa shilingi 60,000 tu kwa mwaka.
Hatua hizi zinadhihirisha juhudi za serikali za kuwekeza kwenye elimu ya amali ili kukuza ustawi wa kijamii na kiuchumi wa nchi kupitia nguvu kazi yenye ujuzi.