Rais William Ruto, mwenyekiti wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ameitisha mkutano wa dharura kujadili vita vinavyozidi kushamiri mashariki mwa Congo.
“Kutokana na hali mbaya ya kibinadamu, inayozidishwa na operesheni za kijeshi zinazoendelea, ikiwemo kufungwa kwa anga ya Goma, natoa wito wa kusitisha mapigano mara moja na bila masharti,” alisema kiongozi huyo wa Kenya katika taarifa yake Jumapili.”Baada ya kushauriana na wakuu wa nchi wa eneo hili kuhusu hali hii ya hatari, tutakuwa na Mkutano Maalum wa Dharura wa EAC ndani ya saa 48 zijazo ili kujadili mgogoro huu na kutoa mwelekeo wa suluhisho.
Hili linaendana na uamuzi wa Mkutano wa EAC wa Novemba 2024 uliotaka mashauriano ya kujenga ili kushughulikia mgogoro huu. Nawashukuru Rais Tshisekedi na Rais Kagame kwa kuthibitisha ushiriki wao katika mkutano huu.”Hatua ya Ruto inakuja wakati kundi la M23 likidai kuwa limeiteka Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini, hali ambayo imesababisha wimbi kubwa la wakimbizi.
Ruto alisisitiza jukumu la pande zote kuruhusu misaada ya kibinadamu kufikia walioathirika na kuhimiza pande zote mbili kutafuta njia za amani za kutatua mgogoro huu wa kusikitisha.”ongezeko la matukio ya kutisha, pamoja na kuongezeka kwa mvutano wa kidiplomasia katika eneo hili, yanashinikiza haja ya haraka ya suluhisho la amani kwa mgogoro unaoendelea kusababisha mateso makubwa kwa watu, hasa wanawake na watoto,” alisema.