Rais wa Zanzibar, Hussein Ali Mwinyi, amezihimiza nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuharakisha uanzishwaji wa mfuko maalum wa mafuta na gesi ili kukabiliana na changamoto za kifedha na kuharakisha maendeleo ya sekta hiyo katika kanda.
Akizungumza katika hafla ya kufunga Mkutano na Maonesho ya 11 ya Mafuta na Gesi Afrika Mashariki 2025 (EAPCE 25) jijini Dar es Salaam, ambayo ilikusanya zaidi ya wadau 1,400 kutoka ndani na nje ya kanda, Dk. Mwinyi alisisitiza umuhimu wa kuwa na uhuru wa kifedha katika kutekeleza miradi ya mafuta na gesi.”Ukosefu wa fedha za kutosha umeendelea kuwa kikwazo kikubwa katika sekta ya mafuta na gesi ya kanda hii.
Kuanzisha mfuko wa mafuta kutatusaidia kukabiliana na changamoto za kifedha zinazosababishwa na harakati za wanaharakati wa kimataifa na mabadiliko ya vipaumbele vya wafadhili wa jadi,” alisema.Dk. Mwinyi alibainisha kuwa wanaharakati wa mazingira duniani kote wamekuwa wakishinikiza taasisi za kifedha kusitisha ufadhili wa miradi ya mafuta na gesi, jambo ambalo limeifanya iwe vigumu kwa mataifa ya Afrika kupata rasilimali kwa ajili ya miradi yao ya nishati.
Katika kipindi ambacho wanaharakati wa kimataifa wanazidisha upinzani wao dhidi ya ufadhili wa miradi ya mafuta na gesi, huku taasisi za mikopo ya kuuza nje zikionyesha kusita kusaidia miradi hiyo, tunapaswa kujiuliza: Je, sisi kama nchi wanachama tunakabiliana vipi na changamoto hizi? Tunawezaje kushinda vikwazo hivi ili kuendeleza rasilimali zetu za mafuta na gesi na kutekeleza mipango yetu ya mpito wa nishati kwa ufanisi?” aliuliza.
Kauli yake inahusiana na upinzani uliowahi kukumba mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), ambao ulikutana na upinzani mkali kutoka kwa makundi ya wanaharakati wa mazingira nchini Ufaransa na sehemu nyingine za dunia.Dk. Mwinyi alitaja Umoja wa Wazalishaji wa Mafuta wa Afrika (APPO) na Benki ya Afrika ya Maendeleo ya Biashara (Afreximbank) kama mifano ya jinsi ya kupata ufadhili endelevu kwa sekta hiyo.