Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amezungumza na Elon Musk kuhusu suala la upotoshaji wa habari kuhusu Afrika Kusini, ikulu ilisema Jumanne, baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kusema kwamba atasitisha msaada kwa nchi hiyo kutokana na sera yake ya mageuzi ya ardhi.
Trump Jumapili alishutumu Afrika Kusini kwa kunyang’anya ardhi na kuwadhulumu “makundi fulani ya watu”. Ramaphosa alijibu Jumatatu kwamba serikali haijachukua ardhi yoyote kwa nguvu na kwamba sera hiyo inalenga kuhakikisha upatikanaji wa ardhi kwa usawa kwa umma.
Tajiri mzaliwa wa Afrika Kusini, Elon Musk, ambaye ni rafiki wa karibu wa Trump, aliingilia mjadala huo Jumatatu kwa chapisho kwenye X akidai kuwa Afrika Kusini ina “sheria za umiliki wa ardhi zilizo wazi za kibaguzi”, akidokeza kuwa watu weupe ndio waathirika.
Ikulu ilisema kwenye X kwamba Ramaphosa na Musk walizungumza Jumatatu “kuhusu masuala ya upotoshaji wa habari na upindishaji wa ukweli kuhusu Afrika Kusini. Katika mazungumzo hayo, Rais alisisitiza thamani za katiba ya Afrika Kusini zinazohimiza heshima kwa utawala wa sheria, haki, usawa na usawa kwa wote,” lisema, bila kutoa maelezo zaidi.