Awali tarehe 11 Okotoba mwaka 2024, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilifahamisha umma kuhusu zoezi la kuondoa kwenye mzunguko noti za zamani za Shilingi 20, 200, 500, 1000, 2000, 5000 na 10000 kwa matoleo ya mwaka 1985 hadi mwaka 2003 na noti ya 500 iliyotolewa mwaka 2010 zenye sifa zilizoainishwa kwenye tangazo la Serikali Na. 858.
Zoezi la ubadilishwaji wa noti hizo limeanza tarahe 6 Januari 2025 na litamalizika tarehe 5 April 2025 kupitia ofisi za Benki Kuu na benki zote za biashara kwa kupatiwa malipo yenye thamani sawasawa na kiasi kitakachowasilishwa.
Aidha baada ya muda huo kupita matumizi ya fedha hizo yatafika ukomo wa kuwa fedha halali za Tanzania hivyo mtu yeyote au taasisi yoyote inayomiliki noti hizo za zamani haitaruhusiwa kutumia noti hizo vilevile benki zote hazitaruhusiwa kupokea amana au maombi yakubadlishwa noti zilizoondolewa kwenye mzunguko.
Hivyo Benki Kuu inawaomba wananchi wote wenye akiba ya noti hizo za zamani kuzibadilisha au kuziweka amana kwenye benki ndani ya kipindi husika kilichotolewa.