Benki ya NMB imeandika historia ya kuwa Taasisi ya kwanza nchini Tanzania kutambuliwa na shirika la Top Employers la nchini Uholanzi kama mwajiri kinara wa Tanzania. Taasisi hiyo imezawadia tuzo mashirika mbalimbali kwenye nchi 124.
Taarifa hizi zinakuja baada ya NMB kutunukiwa tuzo ya mwajiri bora wa Tanzania mwaka 2023 na mwajiri bora Afrika mwaka 2022 ikithibitisha nafasi yake kama kiongozi wa ajira bora.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Afisa Mkuu wa Rasilimali Watu wa NMB Bw. Emmanuel Akonaay amesema tuzo hiyo ni ushahidi wa juhudi za benki hiyo kuboresha mazingira ya kazi maendeleo ya wafanyakazi takriban 4000.
Aidha kwa upande wa NMB wameahidi kuwekeza kwa wafanyakazi wake kwa lengo la kukidhi mahitaji yanayobadilika ya ulimwengu wa kazi ambapo Bw. Emmanuel Akonaay amesema kuwa benki hiyo itaendelea kubuni mbinu bora za ajira na kukuza utamaduni wa kazi unaochochea ukuaji wa kitaaluma na maendeleo binafsi ya wafanyakazi wake akisisitiza kuwa mafanikio hayo ni chachu ya kuimarisha nafasi ya NMB kama kinara wa huduma za kifedha na mazingira bora ya kazi.