Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, ametoa maelekezo kwa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Rukwa kuhakikisha wanatunza na kuhifadhi rasilimali za maji na vyanzo vyake, ikiwemo kutoa elimu ili huduma za maji ziwe endelevu.
Ametoa maelekezo hayo, wakati wa ziara yake ya kikazi aliyoifanya leo baada ya kuzindua miradi ya maji katika vijiji vya lleya na Sambewe, wilayani Mbozi, mkoani Songwe.
Akizungumza na viongozi na wananchi wa vijiji hivyo, Mhandisi Kundo amekiri kuwepo kwa changamoto ya maji ambapo katika Kata ya Itumpi, Kundo amesema Serikali imeshafanya ufumbuzi wake kwa kujenga miradi ya maji inayogharimu shilingi milioni 120.
Miradi hiyo ya maji imehusisha, uchimbaji wa visima viwili vyenye uwezo wa kuzalisha lita 4,800 na 6,200 kwa saa, ujenzi wa matenki mawili kwa ajili ya usambazaji, pamoja na vituo vinne vya kuchotea maji.
Kundo pia amepongeza mamlaka za maji Wilaya ya Mbozi kwa usimamizi mzuri wa miradi hiyo na jitihada za kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati.
Aidha, amewashukuru wananchi wa vijiji vya lleya, Sambewe kwa ushirikiano wao katika utekelezaji wa mradi.Awali katika taarifa yake, Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Mbozi, Ismail Nassor, amesema miradi hiyo ya maji itahudumia wakazi 4,068 wa vijiji vya lleya na Sambewe.