Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt.Doto Biteko amesema kuwa maandalizi ya Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika wenye lengo la kuharakisha upatikanaji umeme kwa Waafrika milioni 300 ifikapo 2030 (Mission 300) utakaofanyika tarehe 27 na 28 Januari jijini Dar es Salaam yamefikia asilimia 95.
Dkt. Biteko amesema hayo tarehe 15 Januari 2025 mara baada ya kukagua maandalizi ya Mkutano huo katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam akiwa ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila.
Amesema Wakuu wa Nchi 54 kutoka Bara la Afrika wanatarajiwa kushiriki pamoja na viongozi wengine ambao ni Mawaziri wa Fedha na Nishati kutoka barani Afrika, Marais wa Benki ya Dunia (WB) na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), pamoja viongozi kutoka Jumuiya ya Ulaya na Jumuiya ya Umoja wa Afrika
Huku kazi zinazoendelea kwa sasa ni pamoja na kukamilisha ukarabati wa ukumbi wa JNICC.”Kazi nyingine zinazoendelea ni pamoja na usajili na uthibitisho wa wageni ambao watakuja kwa ajili ya ushiriki na ukarabati wa maeneo mengine yatakayotumika kwenye mkutano huu, nichukue nafasi hii kuupongeza uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa hatua iliyofikiwa na kuliweka jiji kwenye mandhari ya kuvutia.” Amesema Dkt. Biteko