Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) yatangaza uwepo wa Kimbunga ‘JUDE’ katika Bahari ya HindiMamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetangaza uwepo wa Kimbunga ‘JUDE’ katika Bahari ya Hindi karibu na Mfereji wa Msumbiji, ikionya kuwa kinaweza kuathiri mifumo ya hali ya hewa na kusababisha ongezeko la mvua katika baadhi ya maeneo ya nchi.
Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu, Machi 10, 2025, TMA ilieleza kuwa tathmini ya mifumo ya hali ya hewa inaonyesha kuwa kimbunga hicho kinatarajiwa kufika pwani ya Msumbiji baadaye leo kabla ya kudhoofika.”Kimbunga ‘JUDE’ kinatarajiwa kurejea baharini na kupata nguvu tena kati ya Machi 13 na 15, 2025.
Hata hivyo, kutokana na mwelekeo wake na umbali wake wa sasa, hakitarajiwi kuwa na athari za moja kwa moja kwa Tanzania,” sehemu ya taarifa hiyo imeeleza.TMA imeongeza kuwa uwepo wa kimbunga hicho katika Mfereji wa Msumbiji unatarajiwa kuathiri mifumo ya hali ya hewa nchini, hali inayoweza kusababisha ongezeko la mvua katika maeneo mbalimbali.
Maendeleo haya yanatokea wakati wa msimu wa Mvua za Masika, msimu ambao huathiri maeneo yanayopata vipindi viwili vya mvua kwa mwaka.
Mamlaka imewashauri watumiaji wa bahari na wananchi kwa ujumla kufuatilia taarifa za hali ya hewa na kufuata ushauri wa wataalamu husika.”TMA inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa Kimbunga ‘JUDE’ na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa nchini. Taarifa za maendeleo zitatolewa kadri itakavyohitajika,” taarifa hiyo imehitimisha.