Kampuni ya kubadrirsha fedha ya Bybit yenye makao yake Dubai imethibitisha wizi wa rekodi wa pesa za kidijitali (crypto).Walaghai wanasadikika waliweza kufikia pochi za mtandao wa thamani ya pauni bilioni 1 na kuhamisha mali hizo kwa anwani isiyojulikana.
Kampuni ya uchanganuzi wa blockchain, Arkham Intelligence, imeituhumu kundi la wadukuzi wa Korea Kaskazini linalojulikana kama Lazarus Group kwa kuhusika na udukuzi huo.Kampuni hiyo ilichapisha kwenye mitandao ya kijamii kwamba mmoja wa wachunguzi wao wa mtandaoni aliwapatia “uthibitisho wa wazi” kuwa washambuliaji hao walikuwa kutoka kwa kundi hilo hatari la Korea Kaskazini.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Bybit, Ben Zhou, alisema kuwa kampuni yake ilipokea zaidi ya maombi 350,000 ya uondoaji wa pesa baada ya shambulio hilo.Bybit, iliyoanzishwa mnamo 2018, inashikilia mali ya thamani ya pauni bilioni 15 na inawapa watumiaji wake huduma mbalimbali za sarafu ya kidijitali.
Shambulio hili la pauni bilioni 1 lilisababisha thamani ya Ethereum kushuka kwa takriban asilimia nne siku ya Ijumaa.Mnamo mwaka wa 2024, Korea Kaskazini irilipotiwa kuiba takriban dola milioni 800 kwa njia ya crypto, kulingana na taarifa za Redbord.Mnamo 2022, ilikadiriwa kuiba dola bilioni 1.7 kwa mujibu wa jukwaa la ujasusi wa vitisho, linalofahamika kwa jina la Recorded Future.
Mashambulizi mengine makubwa ya pesa za kidijitali hapo awali yamesababisha upotevu wa mamia ya mamilioni ya pauni zikichukuliwa kutoka kwa pochi za watu mtandaoni.
Mnamo 2019, takriban pauni milioni 32 za Bitcoin ziliibwa kutoka katika soko la Binance.Jukwaa hilo lilisema kuwa wadukuzi waliiba zaidi ya Bitcoin 7,000 na kutekeleza “uvunjaji mkubwa wa hali ya usalama wa fedha za kidijitali.”