Ontario imetangaza mpango wa kuweka ushuru wa asilimia 25 kwenye umeme unaouzwa kwa baadhi ya majimbo ya Marekani kuanzia Jumatatu, ikiwa ni hatua ya kulipiza kisasi dhidi ya ushuru wa asilimia 25 uliowekwa na Rais Trump kwa bidhaa za Canada. Hatua hii inatarajiwa kuathiri takriban Wamarekani milioni 1.5 katika majimbo kama Michigan, New York, na Minnesota.
Shirika la North American Electric Reliability Corporation (NERC) limeeleza wasiwasi wake kwamba vikwazo kwenye biashara ya umeme na gesi kati ya Canada na Marekani vinaweza kuhatarisha uthabiti wa gridi ya umeme kwa pande zote mbili. Ingawa biashara ya umeme kati ya nchi hizo mbili ni ndogo,ila ina umuhimu mkubwa katika kusawazisha upatikanaji wa nishati.
Hata baada ya Rais Trump kuchelewesha maamuzi baadhi kuhusiana na ushuru wa bidhaa kutoka Canada kwa mwezi mmoja, Canada bado imesalia na ushuru wake wa kulipiza kisasi kwa bidhaa mbalimbali kutoka Marekani, ukiwemo ushuru mpya wa umeme kutoka Ontario.
Wataalamu wanatahadharisha kuwa ushuru huu unaweza kusababisha kupanda kwa bei ya umeme katika majimbo yanayoathirika, ingawa upatikanaji wa nishati hauwezi kuathirika mara moja.
Kwa mfano, jimbo la Connecticut hupata takriban asilimia 5 ya umeme wake kutoka Canada, na vyanzo mbadala kama gesi asilia vinaweza kusaidia, lakini navyo vitaathirika na ushuru huu mpya.
Hali hii inaonyesha uhusiano wa karibu wa nishati kati ya Canada na Marekani, ambapo mgogoro wowote unaweza kuathiri uchumi wa nchi zote mbili.