Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Benki ya Dunia zimeahidi kwa pamoja dola bilioni 40 kwa mpango wa “Mission 300,” ambao unalenga kuwapatia umeme watu milioni 300 barani Afrika ifikapo mwaka 2030.
Akizungumza kwenye Mkutano wa Afrika wa Mission 300, Rais wa AfDB, Dkt. Akinwumi Adesina, alisisitiza jukumu muhimu la nishati katika kukuza uchumi wa Afrika. Alibainisha kuwa ukosefu wa upatikanaji wa umeme unapunguza pato la ndani (GDP) la bara hili kwa asilimia 2 mpaka 4 kila mwaka, na hivyo kudhoofisha juhudi za maendeleo.
“Tangu AfDB ilipozindua Mpango Mpya wa Nishati kwa Afrika mwaka 2016, kumekuwa na maendeleo makubwa,” Dkt. Adesina alisema mbele ya viongozi wa mataifa na serikali. “Asilimia ya watu barani Afrika wenye umeme imeongezeka kutoka asilimia 39 mwaka 2015 hadi asilimia 52 mwaka 2024.”Licha ya mafanikio haya, pengo la nishati barani Afrika bado ni kubwa, ambapo zaidi ya watu milioni 571 bado hawana umeme sawa na asilimia 83 ya watu wote ulimwenguni wasio na umeme.
Aidha, zaidi ya Waafrika bilioni moja hawana suluhisho safi za kupikia, changamoto ambayo inaathiri zaidi wanawake na watoto.”Lazima tuchukue hatua madhubuti kupunguza takwimu hizi,” Dkt. Adesina alisisitiza.
Alitangaza kuwa mpango wa Mission 300, uliozinduliwa kwa kushirikiana na Rais wa Benki ya Dunia, Ajay Banga, unalenga kuziba pengo hili na kuleta mapinduzi katika sekta ya nishati barani Afrika.AfDB imejitolea kutoa dola bilioni 18.2 kwa mpango huo, huku Benki ya Dunia ikiahidi dola bilioni 22.