Tangu kuanzishwa kwa ubia wa Twiga na serikali ya Tanzania mwaka 2019, Kampuni ya Barrick Gold Corporation imewekeza zaidi ya Sh trilioni 10.1 katika uchumi wa Tanzania.
Kampuni hiyo ya madini, katika taarifa yake, ilieleza kuwa mnamo mwaka 2024 pekee, ubia huo ulichangia Sh trilioni 2.1, jambo linaloangazia mchango mkubwa wa Twiga, ambao unasimamia migodi ya dhahabu ya North Mara na Bulyanhulu, katika kukuza uchumi wa taifa.
Rais na Mtendaji Mkuu wa Barrick, Mark Bristow, alisisitiza kuwa ushirikiano wa Twiga umejidhihirisha kuwa kiongozi katika sekta ya uchimbaji madini nchini Tanzania.
Alieleza kuwa mpango huo haujaishia tu kuunda maelfu ya ajira bali pia umechangia kwa kiasi kikubwa kusaidia biashara za ndani na kufadhili miradi inayolenga kuboresha maisha ya Watanzania.
Sehemu muhimu ya mafanikio ya Barrick nchini Tanzania imekuwa ni msisitizo wake katika matumizi ya bidhaa na huduma za ndani. Mnamo mwaka 2024, kampuni hiyo ilitumia Sh trilioni 1.3 kwa wasambazaji na watoa huduma wa ndani, sawa na asilimia 83 ya matumizi yake yote nchini.
Kilicho muhimu zaidi, kampuni hiyo ilisema, asilimia 75 ya malipo kwa wasambazaji yalienda kwa kampuni za wazawa, kiwango kilichozidi lengo la asilimia 61.
“Mbinu yetu siku zote imekuwa ni kutoa kipaumbele kwa ajira za wenyeji na maendeleo yao,” alisema Bristow, akibainisha kuwa asilimia 96 ya wafanyakazi 6,185 wa Barrick ni raia wa Tanzania, huku asilimia 53 wakitoka katika jamii zinazozunguka migodi hiyo.
Kwa mujibu wa Bristow, Barrick pia iliendeleza ahadi yake ya uwajibikaji kwa jamii kwa kuwekeza zaidi ya Sh bilioni 12 katika huduma muhimu kama vile maji safi, huduma za afya, na elimu mnamo mwaka 2024.