Naibu Katibu Mkuu wa baraza la Waislam Tanzania (Bakwata) Sheikh Mohammed Khamis ametoa wito kwa Tume ya Mipango inayosimamia uandishi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kuhakikisha inazingatia na kufanya tathmini ya changamoto zote zilizojitokeza wakati wa Dira ya 2025 zisijirudie kwenye Dira ya 2050.
Ameyasema hayo katika mkutano wa umoja wa taasisi za dini Tanzania uliofanyika Kurasini Jijini Dar es Salaam.
“Changamoto zilizojitokeza kwenye Dira 2025 ni pamoja na kutofungamana kwa sera mbalimbali, ikiwemo sera ya vyama vya siasa na Dira 2025, jambo hili limesababisha kukosekana kwa vipaumbele vikuu vya Taifa kutokana na tofauti iliyopo kati ya sera, ilani za vyama vya siasa na Dira 2025,” alisema Sheikh Khamis.