Kiongozi mkuu wa 49 wa Madhehebu ya Shia Ismailia na mwanzilishi wa Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN), Mtukufu Aga Khan, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 88 jijini Lisbon, Ureno.
Mtukufu Aga Khan, anayefahamika kama Karim Al-Hussaini Aga Khan IV, alijulikana kwa mchango wake mkubwa katika kuboresha ustawi wa binadamu kupitia miradi mbalimbali duniani.
Katika maisha yake, Aga Khan IV alisisitiza Uislamu ni imani inayohimiza kujitolea, uvumilivu, na utu wa mwanadamu mbali na uongozi wa kidini, alihimiza maendeleo ya jamii kupitia sekta za afya, elimu, habari, utamaduni, na ustawi wa jamii.
Alianzisha miradi kama Shule na Chuo Kikuu cha Aga Khan, Mfuko wa Maendeleo ya Kiuchumi wa Aga Khan (AKFED), na Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN), ambao umeleta maendeleo katika afya, elimu, na uchumi, hasa Afrika Mashariki. Nchini Tanzania, mchango wake unaonekana kupitia Mwananchi Communications Limited (MCL) na Hospitali za Aga Khan.