Serikali imeeleza dhamira ya kutenga fedha kwa ajili ya kufadhili wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo ya sayansi, ili waweze kupata nafasi ya kusomea Sayansi na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) nchini Ireland, ambako kuna utaalam wa hali ya juu katika sekta hiyo.
Hayo yamesemwa tarehe 16 Machi, 2025, jijini Dar es Salaam na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya mazungumzo na Waziri wa Nchi wa Maendeleo ya Kimataifa na Diaspora wa Ireland, Mhe. Neale Richard alietembelea Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) na kuona Maabara ya Matumizi Bora ya Nishati Safi.
Prof. Mkenda ameeleza kuwa amemuomba Waziri Neale Richard kushirikiana katika kuwapatia Watanzania ufadhili wa masomo ya TEHAMA nchini Ireland, ili wanapokuwa masomoni waweze pia kufanya kazi katika makampuni makubwa kama Microsoft, Facebook, na mengineyo.
Aidha, Waziri huyo alitoa pongezi kwa DIT kwa kuanza kutekeleza maelekezo ya kuangalia bidhaa ambazo zinaagizwa kwa wingi kutoka nje ya nchi na kuzitengeneza hapa nchini. Hadi sasa, DIT imefanikiwa kuanza kutengeneza vifaa vya bajaji na magari.