Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) kimechukua hatua muhimu katika kupanua uwezo wa Tanzania kuandaa mikutano ya kimataifa kwa kushirikiana na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) katika ujenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mlima Kilimanjaro (MKICC).
Mradi huo, wenye thamani ya zaidi ya Sh385 bilioni, unatarajiwa kuwa kituo kikubwa zaidi cha mikutano katika Afrika Mashariki na Kati pindi utakapo kamilika mwaka 2027.
Makubaliano hayo yalisainiwa tarehe 9 Machi 2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa AICC, Bi Christine Mwakatobe, pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Bw Abdul Razzaq Badru, na yanawakilisha uwekezaji mkubwa katika sekta ya utalii wa mikutano nchini.
Kituo hiki cha kisasa kitajumuisha ukumbi wenye uwezo wa kuchukua watu 5,000, hoteli ya nyota tano yenye vyumba 500, ikiwemo vyumba 10 vya kifahari, eneo la kibiashara lenye ukubwa wa mita za mraba 20,000, maegesho ya magari 2,000, pamoja na sehemu ya kutua helikopta.
Akizungumzia maendeleo hayo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, alisisitiza dhamira ya mkoa huo katika kukitangaza MKICC kama kituo bora cha mikutano ya kimataifa, hatua inayotarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha biashara na diplomasia ya kimataifa.