Young Africans (Yanga SC) wamewasilisha rasmi malalamiko yao kwa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kuhusu kuahirishwa kwa mechi yao ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Simba SC, iliyokuwa imepangwa kuchezwa Machi 8, 2025, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, wakisisitiza kwamba wanapaswa kupewa ushindi.
Aidha, Kamati ya Utendaji ya Yanga SC, chini ya uongozi wa Rais wa klabu Hersi Said, ilifanya kikao cha dharura mtandaoni tarehe 9 Machi 2025 na kufikia uamuzi wa kutoshiriki mechi yoyote ya marudiano kwa mchezo namba 184, bila kujali tarehe mpya itakayopangwa.
Kamati hiyo pia ilieleza kuwa imepoteza imani na Kamati ya Ligi inayoongozwa na Steven Mguto na Katibu wake Almas Kasongo, ikiitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuivunja kamati hiyo na kuteua viongozi wapya, wasio na upendeleo na wenye uwezo wa kusimamia maendeleo ya soka la Tanzania.
Maandalizi ya mechi na ukiukwaji wa kanuni na Simba SCKwa mujibu wa taarifa ya Yanga SC, klabu hiyo ilifuata taratibu zote za maandalizi ya mchezo, ikiwemo kuhudhuria kikao rasmi cha uratibu wa mechi (Match Coordination Meeting – MCM) kilichofanyika Machi 7, 2025, saa 2:00 asubuhi katika Hoteli ya Spice, Dar es Salaam.
Kikao hicho kilihudhuriwa na wawakilishi wa Yanga SC, maafisa wa mechi, maafisa wa usalama, waamuzi wa tathmini, kamishna wa mchezo, pamoja na viongozi wa Bodi ya Ligi.Hata hivyo, katika hali ya kushangaza, usiku wa Machi 7, 2025, Simba SC walifika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa wakiwa na magari kadhaa kwa lengo la kufanya mazoezi ya awali ya mechi.Walifanya hivyo bila kufuata taratibu zinazotakiwa kupata ruhusa kama inavyobainishwa katika kanuni za Bodi ya Ligi.
Hii inajumuisha kuwasilisha maombi yao wakati wa kikao cha MCM na kuwajulisha kamishna wa mchezo, meneja wa uwanja, na timu mwenyeji, Yanga SC,” ilisema taarifa hiyo.