Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha leo Machi 8, 2025 ilipitia shauri la klabu ya Simba kuzuiliwa kuingia kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa kwa ajili ya kufanya mazoezi ya mwisho kuelekea mchezo namba 184 wa Ligi Kuu ya NBC (Young Africans SC vs Simba SC) uliopangwa kufanyika kwenye uwanja huo leo kuanzia saa 1:15 usiku.
Katika shauri hilo, klabu ya Simba iliiandikia barua Bodi ya Ligi kueleza kuhusu tukio tajwa hapo juu, huku pia ikieleza nia yao ya kutoshiriki mchezo huo kwasababu imezuiliwa kutumia haki yao ya kikanuni kama ilivyoainishwa kwenye Kanuni ya 17:45 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Kamati ilibaini pia kuwa walinzi ambao baadhi walifahamika kwa sura kuwa ni wa klabu ya Yanga, walishiriki tukio la kuzuia basi la klabu ya Simba kuingia uwanjani kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:45 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Bodi ya Ligi kupitia Kamati yake ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imeamua kuahirisha mchezo tajwa hapo juu kwa mujibu wa Kanuni ya 34:1 (1.3) ya Ligi Kuu kuhusu Kuahirisha Mchezo, ili kutoa nafasi ya kupata taarifa zaidi zitakazosaidia kufanya maamuzi ya haki.