Meneja Habari na Mawasiliano wa Yanga SC, Ally Kamwe, amekanusha vikali taarifa zinazozunguka kuhusu kufungiwa kwa miaka miwili, akisema kuwa taarifa hizo ni za mitandao tu na kwamba yeye, mawakili wake, wala klabu yake hawajapokea taarifa rasmi kutoka kwa Mamlaka zinazohusika, hususan Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamwe alithibitisha kuwa alialikwa kwenye Kamati ya Maadili ya TFF kutokana na tuhuma zilizotolewa dhidi yake, ambapo alikumbana na shtaka la kudhalilisha mamlaka za TFF na Bodi ya Ligi.
Alieleza kuwa alikutana na mashtaka yanayohusiana na maoni aliyoyatoa kupitia chapisho alilochapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram tarehe 3 Februari 2025. Hata hivyo, alisisitiza kwamba hukumu hiyo haijathibitishwa na mamlaka yoyote rasmi hadi sasa.
Kamwe alisema: “Taarifa za Ally Kamwe kufungiwa miaka miwili ni tetesi, Nasema ni tetesi maana mimi, mawakili wala klabu yangu hatujapewa Taarifa za hukumu hiyo na Mamlaka zinazohusika (Kamati ya Maadili ya TFF), Taarifa hizo ni za mitandao tu.
Akizungumzia kuhusu sababu za kuitwa mbele ya Kamati ya Maadili, Kamwe alisema: “Ni ukweli niliitwa kwenye kamati na shtaka langu niliambiwa kuwa nimedhalilisha Mamlaka kwa maana ya TFF na Bodi ya Ligi kwa kuzungumza maneno ya Uongo yasiyo na busara kwa kutumia chapisho langu kwenye ukurasa wangu wa Instagram ambalo nilichapisha Februari 3, 2025.
Hali hiyo imejenga hisia tofauti miongoni mwa wapenzi wa soka na wadau wa michezo, huku wengi wakiwa na maswali kuhusu utaratibu wa kamati hiyo na kama kuna uhalali wa taarifa hizo zinazozunguka kuhusu adhabu hiyo.
Kamwe amesisitiza kuwa hadi sasa, hakuna taarifa rasmi kutoka kwa mamlaka zinazohusika kuhusu maamuzi yoyote yaliyofanywa dhidi yake