Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mara ya kwanza imepokea Faru weupe 18 kutoka nchini Afrika Kusini kwa lengo la kuimarisha shughuli za uhifadhi nchini.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) ameyasema hayo leo katika hafla ya makabidhiano ya faru hao iliyofanyika katika Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, Mkoani Arusha leo Machi 4,2025.
Mradi wa kupandikiza faru weupe ndani ya hifadhi ya Eneo la Ngorongoro ni jitihada za kuimarisha shughuli za uhifadhi nchini na unatekelezwa kwa mara ya kwanza kupitia makubaliano ya Wizara ya Maliasili na Utalii na kampuni ya And Beyond” amesema Mhe. Chana.
Mhe. Chana amefafanua kuwa katika makubaliano kati ya Wizara ya Maliasili na Utalii na kampuni ya AndBeyond ilichukua jukumu la kuwezesha upatikanaji na usafirishaji faru weupe 18 kutoka nchini Afrika Kusini kwa awamu ya kwanza na awamu ya pili inategemewa kupatikana kwa faru wengine 18 ili kufikisha jumla ya faru 16 ambapo wengine watawekwa katika maeneo mengine ya uhifadhi nchini.
Mhe. Chana amemshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihda za dhati za kukuza na kuimarisha sekta ya uhifadhi ikiwa ni pamoja na mradi huo wa kupandikiza faru weupe.Ameweka bayana kuwa Faru weupe ni moja ya wanyamapori ambao wapo hatarini kutoweka na hivyo kuorodheshwa kwenye makundi ya wanyamapori na mimea inayolindwa na Mkataba wa Kimataifa wa Biashara ya Wanyamapori na Mimea iliyo hatarini kutoweka (CITES).
Kufuatia hatua hiyo amesema kiu ya Tanzania ni kuunga mkono juhudi za nchi nyingine hususan za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kwa kuwahifadhi wanyamapori hawa katika mazingira ya asili tofauti na maeneo mengine ambapo hufugwa katika mashamba maalum au bustani.
Amefafanua kuwa pamoja na mambo mengine Faru weupe watatumika kutoa elimu kwa jamii juu ya usimamizi na uhifadhi wa faru, kuendeleza tafiti zitakazoleta matokeo yatakayoboresha sayansi na uhifadhi wa wanyama hao.