Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Daniel Mushi amesema Serikali inaendelea na jitihada za kuwajengea wataalamu uwezo wa kufahamu vyema sayansi na teknolojia ya nyuklia ili waweze kutumia vyema vifaa vinavyotumia teknolojia ya nyuklia kwa usalama na maendeleo ya nchi.
Prof. Mushi ameyasema hayo Jijini Dar es salaam baada ya kufanya mazungumzo na Katibu Mtendaji wa Mkataba wa kupiga marufuku majaribio ya silaha za nyuklia (CTBTO) Dkt. Robert Floyd ambaye yupo nchini kwa lengo la kutembelea mtambo unaohusika na kung’amua majaribio ya uchafuzi wa anga utokanao na viasili vya mionzi.
Dtk. Floyd ameipongeza Tanzania kwa namna inavyoendesha mtambo wa kung’amua majaribio hatarishi ya silaha za kinyuklia na kuahidi kuongeza wigo wa wataalamu kupata mafunzo ya namna uendeshaji wa kituo na mafunzo ya matumizi ya taarifa za CTBTO kote duniani.
Aidha Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) Prof. Najat Kassim Mohammed amesema kituo cha kung’amua uchafuzi wa majaribio ya nyuklia ni kituo muhimu kwa nchi na taarifa zake huoanishwa na vituo vingine 306 duniani na kutoa majibu kama kuna sehemu kumefanyika majaribio hatarishi ya teknolojia ya nyuklia.
Tanzania ni nchi mwanachama wa Shirika la Nguvu za Atomu duniani (IAEA) ambapo imeridhia mkataba wa Kimataifa wa kupiga marufuku uchafuzi wa hewa utokanao na viasili vya mionzi.
Mkataba wa Kupiga Marufuku Majaribio ya Nyuklia (CTBTO) umekuwa msingi wa juhudi za kimataifa za kuzuia usambazaji na majaribio ya silaha za nyuklia tangu ulipopitishwa mwaka 1996. CTBTO imechangia kwa kiasi kikubwa katika usalama wa Kimataifa, udhibiti wa silaha, na kuzuia maendeleo ya silaha za nyuklia.