Februari 24, 2025 – Kampuni ya Apple imetangaza mpango mkubwa wa kuwekeza dola bilioni 500 nchini Marekani katika kipindi cha miaka minne ijayo. Hii ni moja ya ahadi kubwa zaidi kufanywa na kampuni ya teknolojia kwa uchumi wa Marekani
Apple inapanga kufungua kiwanda kipya chenye ukubwa wa futi za mraba 250,000 katika jiji la Houston, Texas. Kiwanda hiki kitazalisha seva za mifumo yake ya akili bandia (AI) na kinatarajiwa kuanza kazi mnamo 2026. Lengo ni kuhamasisha uzalishaji wa ndani na kupunguza utegemezi wa viwanda vya nje ya nchi.
Apple inapanga kuajiri wafanyakazi 20,000 katika sekta za akili bandia (AI), uhandisi wa chip za silicon, uundaji wa programu, na kompyuta za wingu (cloud )
Apple itaongeza uwekezaji wake katika mfuko wa “Advanced Manufacturing Fund” hadi dola bilioni 10, kusaidia uzalishaji wa ndani na kuimarisha wauzaji wa ndani wa vifaa na teknolojia.
Apple itaongeza matumizi ya chip zinazozalishwa nchini Marekani ili kupunguza utegemezi wa wazalishaji wa nje, haswa kutoka China.
Hatua hii ya Apple inakuja wakati ambapo mvutano wa kibiashara kati ya Marekani na China unaongezeka, na ushuru mpya ukiongezwa kwenye bidhaa zinazoagizwa kutoka China. Kampuni inajaribu kupanua uzalishaji wake ndani ya Marekani ili kulinda shughuli zake na kuendana na sera za serikali za Marekani kuhusu utengenezaji wa ndani.
Uwekezaji huu unatarajiwa kukuza sekta ya teknolojia ya Marekani, kuunda maelfu ya ajira, na kuimarisha ubunifu katika nyanja za akili bandia, vifaa vya elektroniki, na programu. Wachambuzi pia wanaona hii kama mkakati wa Apple kujipanga vyema na serikali ya Marekani.
Apple imesema itatoa maelezo zaidi katika miezi ijayo, ikijumuisha ratiba za miradi na mipango ya ajira zaidi.