Bei ya dhahabu imepanda na kufikia rekodi ya juu ya Sh7.5 milioni kwa wakia moja ya troy mnamo Februari 15, 2025, ikiwa ni kiwango cha juu zaidi kuwahi kurekodiwa, kulingana na viwango vya kubadilisha fedha vya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Ongezeko hilo la Sh1.3 milioni kutoka wastani wa Sh6.2 milioni mnamo Januari 2, 2025, linaonyesha kuongezeka kwa mahitaji ya wawekezaji katikati ya hali ya sintofahamu ya uchumi wa dunia, ikiwemo shinikizo la mfumuko wa bei na kuyumba kwa sarafu.
Licha ya kufikia viwango vipya vya juu, soko la dhahabu linaendelea kuwa na mtikisiko. Baada ya kufikia wastani wa Sh7.46 milioni mnamo Oktoba 31, 2024, bei hiyo imeshuka kidogo na kufikia Sh7.42 milioni kufikia Jumanne, Februari 18, 2025.
Hata hivyo, ikilinganishwa na kipindi kama hiki mwaka jana, ambapo dhahabu ilikuwa Sh5.02 milioni, thamani ya sasa inaonyesha ongezeko la asilimia 49, jambo linaloashiria mvuto unaoongezeka wa dhahabu kama kitega uchumi salama.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba, alisema kupanda kwa bei ya dhahabu ni kielelezo cha mienendo mipana ya kiuchumi, hususan athari za mfumuko wa bei na kushuka kwa thamani ya sarafu, hali inayowafanya watu wengi zaidi kuwekeza katika dhahabu.
“Changamoto za kiuchumi duniani zimeongeza mahitaji ya dhahabu kama rasilimali thabiti. Shinikizo la mfumuko wa bei na kuyumba kwa sarafu ni sababu kuu zinazowasukuma watu kuelekea dhahabu kama njia salama ya uwekezaji,” alisema.
Takwimu za hivi karibuni kutoka soko la dunia la London zinaonyesha kuwa mnamo Februari 15, 2025, bei ya dhahabu ilipanda hadi dola za Kimarekani 2,908 kwa wakia moja, kutoka dola 2,812 mwishoni mwa Januari, ikionesha ongezeko kubwa ndani ya mwezi mmoja tu.
Bw. Tutuba alihusisha kupanda huku kwa bei na mabadiliko katika usambazaji na mahitaji ya madini hayo adimu, ikiwemo upatikanaji wa dhahabu kutoka migodini.
“Changamoto za kimataifa kama vile hali ya kisiasa isiyo thabiti, migogoro ya kiuchumi, na vita vinavyoendelea vimeongeza hali ya sintofahamu katika masoko ya kifedha, na kuwasukuma wawekezaji kutafuta rasilimali salama kama dhahabu,” aliongeza.
Mchambuzi wa masuala ya kifedha, Oscar Mkude, alielezea matukio maalum duniani, hasa nchini Marekani, yanayoweza kuwa na athari kwa mwenendo wa soko.
“Kuporomoka kwa soko la hisa, pamoja na hatua kali zilizochukuliwa na Rais Donald Trump, kumepelekea wawekezaji wengi kuigeukia dhahabu kwa ajili ya usalama wa kifedha,” alisema.