Kutokana na juhudi za utendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) katika kuvutia uwekezaji na kuboresha huduma kwa wawekezaji, kituo hiki kimetunukiwa tuzo mbili za kimataifa kwa mwaka 2024.
Tuzo hizi ni ushuhuda wa mafanikio ya Tanzania katika kukuza mazingira rafiki ya uwekezaji na kutoa huduma bora kwa wawekezaji.Tuzo ya kwanza ni Tuzo ya Taasisi Bora ya Kuvutia Uwekezaji Barani Afrika, iliyotolewa katika Mkutano Mkuu wa Uwekezaji Duniani (World Annual Investment Meeting 2024) uliofanyika Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE). Tuzo hii ni matokeo ya ushindani mkali kati ya taasisi za kuvutia uwekezaji kutoka nchi mbalimbali za Afrika, ambapo TIC ilionyesha umahiri wake wa kipekee.
Tuzo ya pili ni Tuzo ya Taasisi Bora ya Kuvutia Uwekezaji Afrika kwa Matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma, iliyotolewa na Chama cha Taasisi za Kuvutia Uwekezaji Duniani (World Investment Promotion Agencies – WAIPA).
TIC ilishinda tuzo hii kutokana na mfumo wake wa kidijitali unaowezesha wawekezaji kuwasilisha maombi ya Cheti cha Uwekezaji na kukipata kwa haraka kupitia mfumo wa mtandaoni, bila ulazima wa kukutana ana kwa ana na maafisa wa kituo.