Naibu Katibu Mtendaji anayeshughulikia Biashara na Ubunifu, Dkt. Lorah Madete, leo Januari 14, 2025, amefungua kikao kazi maalum cha maandalizi ya ajenda ya tafiti za kimkakati.
Kikao hicho kimefanyika jijini Dodoma kikihusisha wadau mbalimbali, wakiwemo Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa COSTECH, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kutoka Wizara ya Elimu, Wakurugenzi Wasaidizi wa Sera, Tafiti na Ubunifu, pamoja na wajumbe wengine kutoka kada husika.
Akizungumza wakati wa kufungua kikao hicho, Dkt. Madete alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu katika kufanikisha tafiti zitakazosaidia katika utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP III) na maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.”Mwaka 2023, Serikali ilirejesha Tume ya Taifa ya Mipango kwa lengo la kusimamia uchumi wa taifa na kuhakikisha mipango ya maendeleo inaandaliwa na kutekelezwa kwa namna itakayohakikisha ukuaji endelevu wa uchumi.
Mafanikio hayawezi kufikiwa bila ushirikiano wa wadau pamoja na upatikanaji wa taarifa sahihi kwa ajili ya maamuzi na upangaji wa mipango yenye tija,” alisema.
Dkt. Madete alibainisha kuwa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP III) unasisitiza umuhimu wa tafiti huru na bunifu katika kujenga uchumi wa viwanda na ushindani. Alinukuu nyaraka za Mpango huo zinazosema: “Matokeo ya tafiti huru yatasaidia kuimarisha utekelezaji wa Mpango na hatua za kimkakati.”