Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma, amesema kuwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) imepanga kuhakikisha asilimia 80 ya nyimbo zinazopigwa katika viwanja vya ndege nchini zitakuwa za wasanii wa Tanzania na asilimia 20 zikiwa za kimataifa.
Akizungumza katika hafla ya kusaini makubaliano ya matumizi ya muziki wa Tanzania katika viwanja hivyo, Naibu Waziri Mwinjuma (MwanaFA) amesema hatua hiyo inalenga kukuza soko la kazi za wasanii wa ndani na kuwaongezea mapato kupitia matumizi ya kazi zao.
“Hii ni hatua kubwa kuelekea kuhakikisha wasanii wa Kitanzania wanapata nafasi ya kutangaza kazi zao na kunufaika zaidi kupitia jukwaa hili la kipekee,” amesema Mwinjuma ambaye pia ni mwanamuziki.
Aidha, amewataka wasanii wa Tanzania kuendelea kuzalisha kazi zenye ubora wa hali ya juu ili kufikia matarajio ya soko la ndani na la kimataifa, hasa kupitia fursa mpya zinazopatikana katika viwanja vya ndege nchini.