Kamati ya sera ya fedha ya Benki Kuu ya Tanzania imeamua kuendelea na kiwango cha asilimia 6 kwa robo ya kwanza ya mwaka 2025.
Hayo yametolewa na Gavana wa Benki Kuu Tanzania Bw. Emmanuel Tutuba akizungumza na waandishi wa habari kufuatia kikao cha kamati ya fedha kilichofanyika tarehe 7 Januari.
“Uamuzi huo wa kamati wa kutobadili riba ya Benki Kuu unalenga kuhakikisha kiwango cha ukwasi kinaendelea kuwa cha kutosha katika uchumi, kudhibiti mfumuko wa bei kubaki chini ya lengo la asilimia 5 na kuwezesha kuongezeka kwa kasi ya ukuaji wa uchumi kufikia takribani asilimia 5.7 katika robo ya kwanza ya mwaka 2025,” alisema Gavana Tutubi.
Kuhusu mwenendo wa uchumi wa dunia kamati ya sera ya fedha imesema ripoti za shirika la fedha duniani (IMF) na Benki ya Dunia (World Bank) zinaonyesha ukuaji wa uchumi unaokadiriwa kuwa imara katika mwaka 2024.
Aidha mazingira ya uchumi duniani katika robo ya nne ya mwaka 2024 yaliimarika kwa kiwango kikubwa ambapo kasi ya ukuaji wa uchumi iliongezeka, mfumuko wa bei ulipungua katika nchi nyingi na mazingira ya upatikanaji wa fedha kwa riba nafuu katika masoko yaliimarika.